Makala haya yalichapishwa katika gazeti la Mwananchi, Tanzania tarehe 29 Agosti, 2024.
Shimbo Pastory
Ni dhahiri zipo namna nyingi za kusimulia matukio ya zamani: kwa kurudia kilichosemwa au kilichoandikwa kwamba kilitokea kama kilivyo, kwa kushuhudia kilichoonekana au kupitiwa kama kinavyokumbukwa, na pia kwa kuchanganua yale yaliyotokea katika hizo nyakati za kihistoria na kuyatafutia muktadha wenye tija katika nyakazi zetu.
Kwa sasa, haina maana yoyote kukaa na kusimuliana historia ya mambo yaliyotokea nyuma, hasa yale yenye kuleta maumivu ya kijamii, bila kuyatazama kwa mtazamo mpana wenye maono ya mbeleni.
Hii ni nadharia nzuri kuitumia katika kuizungumzia historia pana iliyopo nyuma ya pazia la historia ya utumwa.
Kumbukizi hii ya kimataifa ya kusitishwa kwa biashara za utumwa, ambayo inaadhimishwa duniani kote tarehe 23 Agosti inatupa nafasi ya kulipambanua kwa upana suala hili.
Uthabiti wa taarifa za kihistoria ni muhimu kwa ajili ya kubainisha ukweli, lakini katika kuwajengea hasa vijana na watoto hisia stahiki wanazopaswa kuwa nazo katika kuchanganua utumwa kama historia yao (au historia ya watu wao) tunapaswa kuvuka uwanda huo.
Tunafanya hivyo kwa kupambanua utumwa (wa kihistoria) kwa mtazamo wa kisasa, na tukiwa akilini na malengo ya kuleta matokeo chanya sasa.
Athari za karne nyingi za utumwa wa watu kutoka Afrika, katika mabara ya Mashariki na Magharibi haziwezi kusemwa kwamba ni za kihistoria peke yake. Athari hizo zipo hadi sasa katika maisha ya jamii zetu, katika mifumo yetu ya kujiongoza, na mbaya zaidi katika fikra za watu wengi duniani.
Kati yetu wenyewe waafrika mojawapo kati ya hizo athari ni kuwa na imani ndogo na watu wa Afrika ukilinganisha na wageni.
Hivyo, vijana wanapofundishwa kuhusu historia ya Utumwa, wanapaswa kufundishwa kwamba sio tu janga la kihistoria, bali ni kipande muhimu cha historia ya watu wa Afrika, ambacho hawapaswi kukiruhusu kijirudie katika misha yao na katika kizazi chao.
Tunapaswa kufundishana historia yetu kama watu huru, na tunaojivunia kuwa huru; sio kama watumwa au watu wanaoelekea kuwa watumwa!
Upo pia katika maisha ya siku hizi utumwa mamboleo, njia mbalimbali mpya za kuwagandamiza, kuwatumia, na kuwanyonya watu kwa faida za matajiri wachache.
Suala la utumwa likiongelewa kwa wazi na katika muktadha wa maisha ya leo tutaokoa maisha ya watu wengi.
Historia ya utumwa ni kielelezo dhahiri kwamba bila kujisimamia wenyewe kwa umoja wa nia tunakuwa ni vibaraka wa watu wenye tamaa, ukweli ambao upo wazi hata katika maisha ya kila siku.
Mashujaa wa kuukataa utumwa wanatengenezwa kwa kufundishwa kuwa wao ni watu huru, na daima wanapaswa kutafuta, kutenda, na kudumisha haki.
Ni wazi vizazi na vizazi vinaweza kunyimwa haki moja baada ya nyingine, na kunyanyaswa hadi kupokonywa utu wao, kama tu hawajisimamii wao wenyewe kwa uthabiti wa ufahamu wao kwamba ni watu huru na wenye haki sawa kama watu wengine wote.
Bado tunayo safari ndefu ya kubadilisha fikra zetu kama watu huru, na kuweza kuthamini kile kilicho chetu kama bora zaidi.
Angalia leo waafrika kunavyosujudia vitu vya kigeni, hata kama tunavyo vizuri zaidi nyumbani. Tamaduni zetu, utaalamu wetu wa asili, sanaa zetu, na mambo mengine mengi tunayachukulia sisi wenyewe kama vile sio bora zaidi.
Tumekwua watumwa wa lugha za kigeni pia, kiasi kwamba lugha hizo zimekuwa kipimo, sio tu cha ufahamu, bali ujasiri, usomi, uwezo wa uongozi na utaalamu.
Waafrika wengi kuwabeza na huwadhalilisha Waafrika wenzao wasiozungumza vizuri lugha hizi za kigeni. Utumwa huu wa kisasa ni mbaya zaidi, kwani ni mgumu kuutambua na kuupatia ufumbuzi.
Tuwafundisheni watoto historia za kishujaa, hata katika mambo kama haya yanayoumiza, ili kuwajengea uwezo wa kuwa makini na kujitetea pale wanapoona wanaonewa, kutumikishwa, au kunyimwa haki zao.
Uonevu ambao ni masalia ya vidonda vya kihistoiria bado upo, dhahiri zaidi tunaposafiri katika nchi za watu na kudharauliwa kama watu maskini na tusiowea kuwa na mchango wowote wa maana. Kuvifundisha vizazi vijavyo historia hii kwa mitazamo mpya itawajenga zaidi na kuwapa nguvu ya kushinda vizuizi vya kihistoria.
Shimbo Pastory ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ateneo de Manila, Manila – Philippines, na ni mwandishi wa safu ya Maendeleo ya Jamii katika gazeti la The Citizen. Website: www.shimbopastory.com.